Maria Mtili October 20, 2017
- Malaria ni ugonjwa unaoathiri watu wengi duniani ikiwamo Tanzania. Ugonjwa huo husababisha vifo vya watu takriban milioni 2.7 kote duniani na vingi hutokea barani Afrika. Ugonjwa huo huonekana katika nchi takribani 100 duniani na umeshaleta athari kubwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Ipyana Samson, Mwananchi, [email protected]
Licha ya kiwango cha Malaria kushuka mkoani Mbeya kwa takriban mara mbili ndani ya miaka mitatu, bado ugonjwa huo umeendelea kuwatesa wakazi wa Wilayani Rungwe kutokana na ugonjwa huo kuendelea kuwaathiri zaidi. Ugonjwa huo umetajwa kuwa namba moja unaowatesa wakazi wengi wa wilaya hiyo.
Taarifa kutoka ofisi ya mratibu wa Malaria mkoani Mbeya, zinaonyesha 2014 kulikuwa na wagonjwa 199,367 na miongoni mwao, wagonjwa 255 walifariki dunia, lakini mwaka jana, idadi ya wagonjwa ilipungua na kufikia 98,835 huku vifo vilivyoripotiwa ni 97.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini miongoni mwa watu walioathirika zaidi ni wakazi wa Kata ya Kisegese, Halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe.
Wakazi hao wanasema hutumia fedha nyingi kutibu ugonjwa kwa sababu eneo lao halina huduma za afya.
Watoto chini ya miaka mitano na wajawazito ndiyo waathirika wakubwa, wengi wao hupoteza maisha baada ya kukosa huduma za haraka kwa sababu kata hiyo haina zahanati wala kituo cha afya ambako wagonjwa wangepata huduma ya haraka na hata wafanyakazi wangesaidia kutoa elimu ya namna ya kujikinga na maradhi hayo. Kwa sasa wakazi hao wanasafiri umbali wa hadi kilomita 20 kusaka matibabu wilaya jirani ya Kyela au husafiri zaidi ya kilomita saba zenye milima mikali kwenda katika hospitali ya Itete iliyopo ndani ya halmashauri hiyo.
Hayo yanatokea licha ya Sera ya afya ya 2007 kuelekeza kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata lazima iwe na kituo cha afya.
Kata ya Kisegese ni moja ya kata 13 za Halmashauri ya Busokelo yenye wakazi 10,000 kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya 2012.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisegese, Alex Mwakifwamba (40) anasema mara nyingi wataalamu wanawaambia ugonjwa unaowasumbua zaidi kwenye kata yao ni malaria ambayo inaua watoto wao wengi.
Mwakifwamba anasema ugonjwa wa Malaria utaendelea kupunguza nguvu kazi ya wakazi hao kama Serikali haita chukua hatua ya kutoa elimu. Anasema kata hiyo imezungukwa na mito na madimbwi mengi ambayo yanatuama kipindi cha masika.
Mkazi wa Kijiji cha Ngereka, Tumaini Mwakosya (35) anasema kinacho watesa zaidi ni kutokuwa karibu na huduma za afya ambako wangeweza kupata matibabu ya haraka na elimu ya kutosha juu ya ugonjwa huo.
“Tumekuwa tukipewa vyandarua kila mwaka lakini bado hatuna elimu nzuri ya matumizi sahihi ya vyandarua hivi kwani wengi wetu tukipewa vyandarua tunaenda kuvulia samaki kwenye mito iliyo karibu nasi hapa kama Mto Lufilyo na Mto Kasyabone,” anasema.
Tumaini anaongeza kuwa mbali na kata hiyo kusumbuliwa na ugonjwa wa Malaria kuna magonjwa mengine yanayowanyemelea watu wazima kama kutapika damu mara kwa mara lakini kutokana kutokuwa karibu na wataalamu wa afya wameshindwa kutambua ugonjwa huo unatokana na nini.
Tofauti na wenzao wa vijiji vya jirani ambao hubahatika kupatiwa elimu na wataalamu wa afya wanaowatembelea, wakazi wa kata ya Kisegese wanasema ni nadra kuwaona watalaamu hao.
Mkazi wa kijiji cha Ngereka Stella Kapala (28) anasema wamekuwa watalaamu wa afya hawaji mara kuwapa elimu namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko na ikizingazitia wao wanaishi bondeni hivyo na magonjwa ya mlipuko huibuka mara kwa mara.
Kwa kuwa hakuna zahanati wala kituo cha afya ambacho kingekuwa kinarekodi taarifa za wagonjwa kila siku, imekuwa ni vigumu kwa mamlaka kupata takwimu kamili za magonjwa yanayowatesa wakazi hao.
Hata hivyo, Mganga mkuu wa Halmashauri hiyo Gilbert Tarimo anasema kwa takwimu walizonazo zilizohusisha wakazi wa kata hiyo walioenda kutibiwa kwenye hospitali za wilaya hiyo, malaria bado inawatesa ikilinganishwa na magonjwa mengine.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tarimo, vifo vya watoto chini ya miaka mitano viliongezeka hadi 35 mwaka 2016 kutoka 30 mwaka 2015 huku vifo vya wajawazito vikiwa ni vitano.
“Vifo vya watoto katika kata ya kisegese kwa watoto chini ya miaka mitano vinatokana na ugonjwa wa Maralia na lishe kwani wazazi wengi wamekuwa hawazingatii suala la lishe bora kwa watoto,”anasema Tarimo.
“Idadi ya vifo vya wakina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano vinaweza kuzidi lakini asilimia kubwa wananchi wetu hutibiwa wilaya jirani ya Kyela na kupelekea sisi huku kukosa takwimu kamili ya vifo hivyo.”
Hata hivyo, ikilinganishwa na miaka iliyopita, Mratibu wa Malaria Mkoa wa Mbeya, Salehe Mwango anasema hali ya ugonjwa wa malaria mkoani hapa imezidi kupungua kutokana na juhudi za serikali na kampeni ya tokomeza malaria.
“Ugonjwa wa malaria katika mkoa wetu siyo mbaya sana kwani takwimu zinaonyesha wagonjwa kupungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma,” anasema.
Mwango anasema mwaka 2014 kulikuwa na wagonjwa 199,367 na watu 255 walifariki lakini mwaka jana walishuka hadi 98,835 na vifo 97 tu.
Mwango anasema tangu mwaka 2014 mkoa umejikita kugawa na kuhamasisha wananchi matumizi ya vyandarua wakati wa kulala na mwitikio umekuwa ni mkubwa sana lakini kuna baadhi ya sehemu mwitikio ni hafifu hasa katika Wilaya ya Rungwe na Kyela ndiyo maana wanaendelea kuhamasisha.
Daktari kutoka hospitali ya Rufaa Mbeya, Majuni Mutwagwaba anasema kutokana na hali ya ugonjwa hiyo kuwa mbaya katika kata hiyo kuna haja ya Serikali kupitia halmashauri kuwekeza nguvu kubwa ya kutoa elimu kwa wakazi wa kata hiyo ili kunusuru kizazi kijacho.
“Malaria ni ugonjwa uliyoshika nafasi kubwa katika maeneo mengi nchini hivyo licha ya Serikali kujaribu kudhibiti lakini bado hali ni mbaya kwa wananchi washio vijijini kwani elimu wanayoipata juu ya matumizi sahihi ya vyandarua na kunawa mikono baada kutoka chooni hawaitilii manani,” anasema.
Mutwagwaba anaongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuwa karibu na watalamu wa afya ili kuweza kukomboa kizazi kijacho lakini pia Serikali iweke sheria kali kwa mwananchi ambaye atakuwa hana choo bora na cha kisasa kama Serikali inavyotaka.
Mkurugenzi was asasi ya kiraia ya Mbengonet, Paul Kiita anasema ufwatiliaji wa Serikali umekuwa siyo mzuri kwa wananchi wanaoishi vijijini kwenda kufahamu utekelezaji wa magizo wanayotoa kwa viongozi wao.
“Tatizo hili haliwezi kuisha mapema kama Serikali inatarajia kama haijaweka mkazo juu ya ujenzi wa vyoo bora kwani tatizo kubwa lipo hapo na sisi kama asasi tumepanga kwamba mwakani tutazunguka wilaya zote za Mbeya kutoa elimu juu ya ujenzi wa vyoo bora,” anasema Kiita.