Maeneo 10 ya kutazamwa kufanikisha ukusanyaji mapato ya serikali

Maria Mtili
October 26, 2017

  • 5 tri: Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha uliopita. Kati ya trilioni hizo, utekelezaji haukufika nusu.
  • 10%: Kiwango ambacho Serikali ilishindwa kukusanya kutoka ndani.
  • Sh17t: Kiasi ambacho TRA inapaswa kukusanya mwaka huu wa fedha.

Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]
Wakati Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ikitangaza kuajiri watumishi wapya 400, maeneo kadhaa yanapaswa kupewa kipaumbele kuhakikisha malengo ya ukusanyaji mapato yanafikiwa.

Katika vyanzo 12 vya mapato ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 ambavyo gazeti hili limechunguza, vyote haviku-fikia lengo lililowekwa isipokuwa viwili. Itakumbukwa, bajeti ya mwaka 2016/17 iliongezwa kwa takriban Sh7 trilioni ikilinganishwa na ya mwaka 2025/16.

Kwenye bajeti hiyo ya Sh29.5 trilioni, Serikali ilipanga kukusanya Sh18.465 trilioni kutoka vyanzo vya ndani, lakini juhudi zote zilizoelekezwa katika ukusanyaji zilifanikisha kupatikana kwa Sh16.639 trilioni.
Kutoka vyanzo vyote, vya kodi na visivyo vya kodi, Serikali ilikuwa na nakisi ya asilimia 10 ya matarajio yake (sawa na Sh1.826 trilioni).

Kati ya fedha hizo, vyanzo vya Serikali vilitarajiwa kuingiza Sh17.798 trilioni kwa miezi 12 ya utekelezaji wa bajeti hiyo, lakini ni Sh16.128 trilioni pekee zilipatikana. Serikali haikuweza kukusanya asilimia 9.3 ya ilichotarajia, kiasi ambacho ni sawa na Sh1.67 trilioni.

Huenda eneo hili likaimarika mwaka huu wa fedha baada ya Serikali kuiongea TRA wigo wa kodi, kama kukusanya kodi ya majengo. Itakumbukwa kuwa kodi hiyo ilikuwa inakusanywa na halmashauri, lakini kuanzia Oktoba mosi mwaka ja-na mabadiliko hayo yalifanywa.

Alipokuwa akiwasilisha bejeti ya mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema majiji, manispaa na miji 30 imehusishwa kwenye utekelezaji huo ambao mpaka Mei, TRA ilikuwa imefanikiwa kukusanya Sh15.134 bilioni.
Licha ya kuongeza chanzo hicho, kwenye Sheria ya Fedha mwaka 2017, kazi za wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la wamachinga, washereheshaji, wachimbaji wadogo wa madini na maeneo mengine, zilirasmishwa ili kuifanya Serikali iongeze wigo wa mapato yatokanayo na kodi. Endapo usimamizi utakuwa wa kutosha, wachambuzi wa uchumi wanasema makusanyo yatakuwa ya kuridhisha.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango. PICHA| MAKTABA

Katika hotuba yake, Waziri Mpango alitoa rai kwa wadau wote, hasa wamiliki wa majengo, viongozi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na TRA kushirikiana bega kwa bega uhakikisha wanafanikisha ukusanyaji wa kodi hiyo kwa maende-leo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwenye vyanzo vya mapato hayo, Sh2.718 trilioni zilitarajiwa kutokana na vyanzo visivyo vya kodi huku serikali za mitaa zikitakiwa kukusanya Sh665.414 bilioni. Malengo ya maeneo yote mawili hayakufikiwa.
Mapato ya vyanzo hivi yalipungua kwa asilimia 23 kila kimoja. Zaidi ya Sh646 bilioni hazikupatikana kwenye mapato ya-siyo ya kodi wakati makusanyo ya halmashauri yalikuwa chini kwa Sh153.696 bilioni.

Kodi

Wakati mapato ya jumla yakitarajiwa kuwa hayo, TRA ilipewa jukumu la kukusanya Sh15.079 trilioni lakini ikaweza kukusanya Sh14.055 trilioni, kwa mujibu wa Ripoti ya BoT kwa mwaka ulioishia Juni.

Baada ya operesheni kubwa iliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na TRA, makusanyo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) yalivuka lengo kwa asilimia tatu baada ya kuingiza Sh3.037 trilioni, kwa mujibu wa ripoti hiyo, kutoka Sh2.928 trilioni zilizokusudiwa.

Hali hiyo ilijitokeza katika kodi nyinginezo ambako makusanyo yalikuwa asilimia 103. Hapa, jumla ya Sh1.094 trilioni zilikusanywa ikilinganishwa na lengo lililowekwa la kupata Sh1.061 trilioni.

Makusanyo ya kodi ya mapato yalikuwa chini kwa asilimia tisa baada ya TRA kuwekekewa lengo la kukusanya Sh5.316 trilioni lakini ikamudu kukusanya Sh4.829 trilioni kwa siku zote 365 za utekelezaji wa mpango mkakati waliojiwekea.

Mwaka uliopita, Serikali iliripoti kufungwa kwa biashara kutokana na sababu mbalimbali. Kati ya Julai mpaka Oktoba mwaka 2016, Serikali ilisema takriban biashara 2,000 zilifungwa.

Habari zinazohusiana: 

Kufungwa kwa biashara hizo kunamaanisha kukosekana kwa kodi itokanayo na faida, kupungua kwa mzunguko wa fedha kunakochangiwa na kushamiri kwa uwekezaji na biashara pamoja na kupungua kwa ajira ambayo huongeza mapato ya watumishi.

Mchakato wa kuwaondoa wafanyakazi hewa pamoja na wenye vyeti feki wapatao 18,000 kunaweza kuwa sababu nyingine ya kupunguza mapato hayo kutoka kwa wafanyakazi wa umma ambao takwimu zinaonyesha mpaka mwaka 2014 walikuwa zaidi ya milioni 1.2.

Kwa kipindi hicho, Serikali ilipanga kulipa mishahara Sh6.6 trilioni, lakini iliokoa kiasi kidogo. Ripoti ya BoT kwa mwaka ulioishia Juni, inaonyesha ni Sh6.367 trilioni zilizotumika.

Misaada na mikopo ni maeneo mengine ambayo malengo hayakufikiwa. Mara kadhaa, Serikali iliwahi kusema masharti magumu ya mikopo na kutotimia kwa ahadi za wahisani kulisababisha kutotimia kwa mapato ya eneo hili. Ilisema hayo ilipokuwa ikifafanua kutekelezwa kwa bajeti hiyo kwa zaidi ya theluthi moja tu.

Kwa mwaka huo wa fedha, Serikali ilitarajia kupata misaada ya Sh1.423 trilioni, lakini ilipewa Sh911.977 bilioni ambazo ni pungufu kwa Sh511 bilioni (sawa na asilimia 36).

Hata mikopo haikupatikana yote. Serikali ilitarajia kukopa Sh4.91 trilioni kwamba vyanzo vyenye masharti kutoka nje kiasi cha Sh4.278 trilioni na ndani Sh1.597 trilioni, lakini changamoto zilizojitokeza zilisababisha lengo hilo lisitimie na kupata Sh2.906 trilioni pekee.

Forodha

Bandari ni miongoni mwa maeneo muhimu kwenye mapato ya Serikali. Mwaka wa fedha uliopita Sh5.773 trilioni zilikadiriwa kuwa zingekusanywa kutoka eneo hili lakini ni Sh5.092 trilioni zilizopatikana licha ya juhudi za dhati za Rais John Magufuli kuhakikisha anaondoa malalamiko ya wafanyabiashara wanaoitumia Bandari ya Dar es Salaam.

Mdororo wa uchumi duniani ulielezwa kuchangia kushuka kwa mapato ya bandari hiyo. Zilikuwapo sababu nyingine pia ambazo kamati ya Bunge ya Miundombinu ilizibaini na kuchangia kupungua kwa shehena za mizigo. Miongoni mwake ni  kodi zinazotozwa kwa watoa huduma wa mizigo ya nje na ushindani mkubwa katika kupakua na kupakia mizigo.

Alipokuwa akiwasilisha ripoti hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2016/17, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Norman Sigalla alisema katika Bandari ya Dar es Salaam inachukua siku tisa kukamilisha mchakato huo, bandari nyingine kama Durban ni siku nne tu.

Alizitaja sababu nyingine kuwa ni tozo za kuhifadhi mzigo bandarini hapo na uwapo wa mamlaka nyingi zinazosababisha ucheleweshwaji wa uondoshwaji mizigo bandarini akitolea mfano wa Sumatra, Ewura, Wakala wa Vipimo, TRA, TBS, TFDA na Maabara ya Serikali.

“Sababu nyingine ni kutofautiana kwa tozo za bandari baina ya nchi na nchi ambapo za Tanzania zipo juu,” alisema Dk Sigalla na kumalizia kuwa sababu nyingine ni shehena inayosafirishwa nje ya nchi kupewa siku 30 bila kujali mazingira ya barabara tofauti na bandari nyingine shindani.

Alipendekeza kufanyiwa kazi kwa changamoto hizo kuepuka kuwapoteza wateja wanaotumia bandari hiyo na kuhamia Mombasa – Kenya, Beira – Msumbiji, Durban – Afrika Kusini au Walvis Bay – Namibia ambazo zimeweka mazingira rafiki na kuwavutia wafanyabiashara wengi.

Changamoto nyingine alisema ni kutokuwapo kwa maegesho kwa ajili ya magari yanayoenda kupakia mizigo bandarini.

Maoni ya wadau

Dk Omari Mbura wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS) anasema changamoto zilizopo zinapaswa kushughulikiwa  na ikiwezekana utafiti ufanyike kubaini kwanini malengo hayafikiwi.

“Niliwafika ofisi za TRA Nachingwea, kuna wafanyakazi watatu tu ambao naamini hawatoshi kuhudumia wilaya nzima. Zipo wilaya nyingine zina maofisa biashara wawili, hawawezi kufanya muujiza. Viongozi wa vijiji wajengewe uwezo ili wakusanye mapato kwenye maeneo yao,” anasema.

Kuhusu halmashauri kutofikia malengo, anasema utafiti ufanyike kujua tatizo ni nini huku akishauri mfumo wa utoaji leseni usiwe na vikwazo vitakavyomkatisha tamaa muombaji. “Biashara ndogo zikirasmishwa, kipato cha wananchi kitaimarika na makusanyo ya serikali yataongezeka,” anasema.

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye anasema zipo changamoto mbili ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi haraka kukabiliana na hali iliyopo.

“Kuna (walipakodi wachache) tax base ndogo nchini. Serikali ihakikishe inaongeza uzalishaji viwandani ili kukuza sekta nyingine,” anasema mkurugenzi huyo.

Anafafanua kuwa mahitaji ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) inahitajika pia kudhibiti vitendo vya rushwa miongoni mwa wafanyakazi wasio waaminifu.  “Uchumi wetu ni mdogo. Serikali inajitahidi kubana matumizi lakini vyanzo vya mapato havitoshi. Visipoongezwa, itafika kipindi makusanyo yatagota,” alisema.

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania