Utoaji chanjo ya tetenasi kwa wajawazito washuka

Nuzulack Dausen
October 31, 2017

  • Kiwango cha wajawazito waliopata chanjo hiyo mwaka 2014 kilipungua hadi asilimia 72 kutoka asilimia 85 mwaka 2013.
  • Wataalamu wa afya wanasema chanjo hiyo ni muhimu kuzuia madhara ya kutu kuingia kwenye mzunguko wa damu.

[email protected]
Dar es Salaam. Pamoja na kuongezeka kwa hamasa ya utoaji chanjo nchini, wastani wa kiwango cha wajawazito waliopatiwa chanjo ya tetenasi (TT2+) kwa zaidi ya mara ya mbili imepungua kwa asilimia 15 ndani ya mwaka mmoja, MwananchiData imebaini.
Uchambuzi wa takwimu zilizochapishwa kwenye tovuti huru ya takwimu za umma ya opendata, unaonyesha wastani wa kiwango cha wajawazito waliopatiwa chanjo hiyo kilishuka hadi asilimia 72, mwaka 2014 kutoka asilimia 85 mwaka 2013.
Kiwango hicho kilikuwa chini kwa miaka miwili ya awali kwani hata 2012, asilimia 84.6 walipata chanjo sawa na wajawazito 85 kwa kila 100 waliofika kupatiwa huduma hiyo.
Shirika la Kimataifa la Afya (WHO) linaeleza chanjo hiyo ni muhimu kwa wajawazito na watoto wachanga ili kudhibiti ugonjwa hatari wa Tetenasi unaoathiri mfumo wa neva na kusababisha mauvimu makali kwenye misuli na hatimaye kusababisha vifo. Wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo hautibiki hivyo kinga ya chanjo ni muhimu.
Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizochapishwa pia katika tovuti ya Hurumap, mwaka 2014 wajawazito milioni 1.2 walipata chanjo hiyo zaidi ya mara mbili kutoka wajawazito milioni 1.59 wa 2013.


Hadi sasa, opendata inaeleza takwimu hizo zilizoboreshwa tena Februari mwaka huu, ndizo zilizochapishwa kwa umma kwa ajili ya kufanya tathmini mbalimbali za afya katika utekelezaji wa sera na mikakati ya kuzuia maradhi nchini.

Pamoja na kuwa kiwango cha wajawazito waliopatiwa chanjo hiyo kilishuka, bado kuna mikoa mitano ilikuwa na wajawazito wengi waliopatiwa TT2+ mwaka 2014 kuzidi wastani wa kitaifa wa asilimia 72.
Mikoa iliyoongoza, kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ni Kilimanjaro uliokuwa na wajawazito zaidi ya tisa kwa kila 10 (asilimia 93) waliopata chanjo hiyo Zaidi ya mara mbili ukifuatiwa na Dar es Salaam, Arusha, Rukwa na Mbeya.


Hata hivyo, kuna mikoa iliyokuwa na kiwango kidogo cha wajawazito waliopata TT2+ kwa zaidi ya mara mbili ikiongozwa na Tabora, uliokuwa na wajawazito takriban sita kwa kila 10 (asilimia 56) ukifuatiwa na Singida, Geita, Tanga na Manyara.
Jitihada za Serikali kueleza kwa undani sababu za kushuka kwa kiwango cha wajawazito waliopatiwa chanjo ya tetenasi zaidi ya mara mbili zimegonga mwamba licha ya Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsacris Mwamaja kupokea maswali kwa wiki moja sasa.
Hata wakati chanjo hiyo kwa wajawazito ikionekana kushuka, katika mpango wa maendeleo wa chanjo wa 2016-2020, Serikali inaeleza kiwango cha utoaji wa chanjo ya Tetenasi kwa watoto kimeongezeka kutoka asilimia 79 mwaka 2013 hadi asilimia 93 mwaka 2014.
“Licha ya mafanikio hayo ya utoaji chanjo nchini, bado kuna ongezeko la watoto ambao hawajachanjwa kati ya mwaka 2010 na 2014,” inasomeka sehemu ya mpango huo.
Tangu programu ya chanjo ilivyoanzishwa nchini 1975, Serikali inasema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri zaidi barani Afrika huku ikibainisha chanjo inapewa kipaumbele na Serikali kupitia mkakati wa afya msingi.
“Tangu kuanzishwa kwa mpango wa utoaji chanjo imesaidia kupunguza vifo vya wato wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano. Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 99 kwa waliozaliwa hai 1,000 hadi vifo 45 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai,” inasema sehemu ya mpango wa chanjo uliochapishwa Februari mwaka jana.
Wataalamu wa afya wanasema chanjo ya tetenasi ni muhimu kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kwa kuwa kundi hilo huwa na kinga dhaifu kuliko mengine.
Daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Christopher Peterson anasema chanjo ya tetenasi inasaidia kuua madhara ya kutu kwenye damu ya mwadamu ambayo ikiachwa huathiri mfumo wa damu.
“Tetenasi inaathiri mzunguko wa damu mwilini na kusababisha mwili kufa ganzi na kufanya mgonjwa apoteze fahamu. Hivyo ni bora watu wakapewa chanjo mapema kabla ya kudhurika na kutu kwa kuwa chanjo husaidia kuimarisha kinga ya mwili,” anasema Dk Peterson.
Anasema kwa kuwa haifahamiki ni lini mtu ataathiriwa na tetenasi, ni vyema Serikali ikaendelea kuwekeza katika upatikanaji wa chanjo hiyo kwa watu wote ili kuzuia athari za ugonjwa huo.

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania