Unaweza kutumia haya kupima ukuaji uchumi wa miaka miwili ya JPM

Nuzulack Dausen
November 6, 2017

  • Serikali ya Rais Magufuli ambayo imetimiza miaka miwili madarakani, inahitaji kuwekeza kwa kasi kukuza uchumi wa kitaifa ili kuwanufaisha watu wengi

Mwananchi [email protected]

Rais John Magufuli amemaliza miaka miwili tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na imeahidi kuwa nchi itakuwa na uchumi wa kati ifikapo 2025 kwa kuchagizwa zaidi na ukuaji wa sekta ya viwanda.

Katika mtazamo huo wa “Uchumi wa viwanda”, Serikali ya Magufuli inatarajia kuwa viwanda ndiyo vitakuwa injini kuu ya kukuza sekta nyingine kama kilimo, biashara na kutokomeza ukosefu wa ajira unaolikabili Taifa kwa sasa.

Ndani ya miaka miwili ya uongozi wake, Rais Magufuli amefanya mabadiliko mbalimbali katika jitihada za kukuza uchumi huku sekta ya madini ikifanyiwa mabadiliko makubwa katika kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha Watanzania.

Hata hivyo, kuelewa zaidi safari ya mikakati hiyo ya kiuchumi ambayo baadhi wanaiita kwa Kiingereza ‘Magufulinomics’ kuna umuhimu wa kutazama baadhi ya viashiria muhimu kama kasi ya ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na ukuaji wa deni la Taifa.

Ukuaji wa uchumi

Katika kipindi hicho cha miaka miwili, uchumi umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia saba ambayo imeshuhudiwa kwa takriban muongo mmoja sasa.

Kitabu cha hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016 kinaonyesha ukuaji halisi wa Pato la Taifa (GDP) ulikuwa kwa asilimia saba mwaka jana kiwango ambacho ni juu ya wastani wa ukuaji wa uchumi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mwenendo huo umeendelea kuakisiwa katika takwimu za robo ya pili ya mwaka huu zilizotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) baada ya Pato la Taifa kukua kwa kasi ya asilimia 7.8.

Benki ya Dunia (WB) inaeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za kipato cha chini ulimwenguni ambazo uchumi wake unakua kwa kasi ukitabiriwa kukua hadi asilimia 7.2 mwishoni mwa mwaka huu na hatimaye kufikia asilimia 7.4 miaka miwili ijayo.

“Nchi kubwa zenye kipato kidogo Kusini mwa Bara la Afrika kama Ethiopia na Tanzania zitakua kwa kasi zikichagizwa zaidi na sekta huduma, uwekezaji wa miundombinu na kilimo.

“Hata hivyo, kutokana na kuongezeka madeni itabidi ziongeze bana matumizi, punguza ongezeko la madeni na kuimarisha sera za kujijenga,” inasomeka sehemu ya Benki ya Dunia iliyotolewa Juni mwaka huu.

Pamoja na mwelekeo mwema wa ukuaji wa uchumi, sekta ya kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 70 ya watu inakua kwa wastani wa asilimia nne chini ya wastani wa kitaifa kwa mwaka, jambo linalofanya wananchi wengi wasiguswe na ukuaji huo wa uchumi.

Tofauti na shughuli za fedha na bima, ujenzi, habari na mawasiliano zilizokua kwa zaidi ya asilimia 10 ndani ya miaka mitatu iliyopita, kasi ya kukua kwa sekta ya kilimo imezidi kushuka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2014 hadi asilimia 2.1 mwaka jana, kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi wa Taifa mwaka 2016.

Hii ina maana kuwa, Serikali ya Magufuli inahitajika kuwekeza kwa kasi kukuza kilimo kizidi wastani wa ukuaji wa uchumi wa kitaifa ili kuwanufaisha watu wengi zaidi wanaotegemea mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Mfumuko wa bei

Kasi ya kupanda kwa bidhaa na huduma imeendelea kuwa ndani ya tarakimu moja kwa kipindi cha miaka miwili ya Magufuli ikiendana na malengo ya Ilani ya CCM.

Hata hivyo, utawala wa Rais Magufuli ulianza kwa kupaa kwa bei za bidhaa na huduma baada ya kasi ya mfumuko wa bei kuongezeka hadi asilimia 6.6 kwa mwaka ulioishia Novemba kutoka asilimia 6.3 Oktoba 2015. Sehemu kubwa ya bidhaa zinavyofanya wananchi watoboe mifuko yao zaidi kuzinunua mara nyingi kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) ni vyakula na vinywaji visivyo na kilevi.

Deni la Taifa

Pamoja na Serikali kuendelea kusaka vyanzo vyake vya mapato kugharamia miradi ya maendeleo, deni la Taifa bado limeendelea kukua ndani ya miaka miwili iliyopita.

Katika kipindi cha mwaka mmoja tu, ripoti ya tathmini ya uchumi ya Agosti inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa deni hilo lilipaa kwa asilimia 14 hadi Sh54.69 trilioni Julai mwaka huu kutoka Sh47.87 trilioni kipindi kama hicho mwaka jana.

Pamoja na kuwa deni hilo linahusisha sekta binafsi, Serikali ndiyo mkopaji mkuu.

BoT inaeleza kuwa kukua kwa deni la nje lililofikia Dola za Marekani 18.91 bilioni hadi Julai mwaka huu kulichagizwa na mabadiliko katika utoaji wa fedha na gharama za kubadilisha fedha kwa kuwa madeni yote yanatozwa kwa Dola ya Marekani.

Uchambuzi unaonyesha deni hilo sasa ni takriban asilimia 50 ya Pato la Taifa (GDP) ambalo ripoti ya mwaka ya BoT ya mwaka 2016 ilikadiria kuwa lilifikia Sh103.7 trilioni.

Hii ni kinyume na makadirio ya Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) ambalo lilikadiria kuwa deni hilo lingefikia asilimia 38 ya Pato la Taifa.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti Serikali imesema inaendelea kulipa madeni mbalimbali na kwa mujibu wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18 takriban Sh9.5 trilioni zitatumika kulipia deni la Taifa.

Mazingira ya ufanyaji biashara

Moja ya ahadi kubwa ya Rais Magufuli kwa Watanzania na wawekezaji wakati wa kampeni mwaka 2015 ilikuwa kuboresha mazingira ya biashara kwa kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikisababisha wafanyabiashara watumie gharama kubwa kuendesha biashara huku baadhi wakikata tamaa.

Moja ya vipimo vinavyoweza kutumika kupima kipengele hicho muhimu kwa ukuaji wa sekta zote nchini ni kipimo cha urahisi wa kufanya biashara kinachotolewa kila mwaka na Benki ya Dunia na hupewa jina la mwaka unaofuata (Ease of doing business report, DB).

Serikali ya awamu ya tano ilianza kwa kufanya vyema baada ya kupanda kwa nafasi saba duniani hadi nafasi ya 132 mwaka 2017 kutoka 139 ya ripoti ya mwaka wa awali baada ya kufanya mabadiliko makubwa katika ufanyaji biashara yakiwemo kuongeza wigo wa ukopaji na taarifa za wakopaji.

Ripoti mpya iliyotolewa Oktoba 31 ya ‘Urahisi wa kufanya biashara 2018’ (DB 2018) Tanzania imeporomoka tena hadi nafasi ya 137 kutoka 132 ile ya mwaka jana, sababu kubwa ikiwa ni kutokana na kuporomoka katika vipengele vya urahisi wa kusajili majengo na ulipaji kodi.

“Tanzania ilifanya usajili wa mali kuwa ghali sana baada ya kuongeza ada ya kusajili ardhi na majengo,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo licha ya kubainisha alama za kuelekea urahisi wa kufanya biashara ziliongezeka kiduchu kwa asilimia 0.11.

Hata hivyo, ripoti hiyo ilionyesha kulikuwa na maboresho makubwa katika kipengele cha urahisi wa kupata vibali vya ujenzi kwa asilimia 4.76 na kufuatiwa na maboresho madogo katika uanzishaji biashara, upatikanaji wa umeme, na mchakato wa ufilisi unaohusisha muda, gharama na matokeo kwa taasisi za ndani zinazotambulika kisheria.

Uboreshaji wa mazingira ya biashara unachochea uwekezaji na kukua kwa ajira nchini jambo litakalochochea mafanikio ya uchumi wa viwanda ambao Rais Magufuli anaupigania usiku na mchana.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania