Watoto yatima wanavyofaidi fursa za elimu

Maria Mtili
November 14, 2017

  • Ni wale wanaotoka katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi yatima

Nuzulack Dausen, Mwananchi [email protected]

Katika kipindi ambacho baadhi ya watoto wenye wazazi wote wakideka na kupata mahitaji yote ya kifamilia na  fursa za elimu,  kuna watoto yatima zaidi ya 700,000 wanaosoma shule za msingi nchini wakiwa hawana uhakika wa kupata huduma za msingi.

Uchambuzi wa takwimu za msingi za elimu Tanzania mwaka 2016 (Best 2016) uliofanywa na gazeti hili unaonyesha  kuwa Tanzania ina watoto yatima 731,536 ambao wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili ikiwa ni sawa na watoto takriban tisa kwa kila 100 wa darasa la kwanza hadi la saba.

Mikoa yenye kiwango kikubwa cha watoto yatima nchini ni Iringa yenye watoto 14 kwa kila 100 (asilimia 14.4) ikifuatiwa na Njombe watoto 13 (asilimia 12.7), Mbeya watoto 11 na Pwani watoto 10 kwa 100 ambayo ni sawa na asilimia 10.4.

Hata hivyo, ipo baadhi ya mikoa yenye kiwango kidogo cha wanafunzi yatima ikiwa ni chini ya wastani wa kitaifa wa watoto tisa kwa kila 100 (asilimia 8.5). Mikoa hiyo ni pamoja na Manyara, Kigoma, Singida, Mtwara na Lindi.

Katika kundi hilo la wanafunzi yatima, takriban robo au asilimia 23 wamepoteza wazazi wote wawili, hivyo kutegemea zaidi msaada wa walezi au wasamaria wema.

Mbali na yatima wa darasa la kwanza hadi la saba, kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa mapema mwaka huu kuna wanafunzi wa elimu ya awali 125,141 ambao wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili, huku zaidi ya theluthi mbili wakiwa ni wale wenye mzazi mmoja.

Mwanza inaongoza kwa kuwa na yatima wengi katika elimu ya awali kwa kuwa na  watoto 10,848 ikilinganishwa na Katavi yenye wanafunzi yatima 1,168.

Wadau wa malezi na haki za watoto, wanaeleza kuwa yatima ni miongoni mwa makundi ya watoto walio hatarini kutengwa katika jamii na kukosa fursa muhimu katika maisha zikiwemo za kielimu, kijamii na kiafya.

Asasi ya kiraia ya Save the Children inaeleza kuwa pamoja na kwamba hawajafanya utafiti kujua chanzo halisi kilichosababisha baadhi ya mikoa kuwa na yatima wengi, tafiti nyingine zilizowahi kufanywa zinaonyesha vyanzo vikuu ni umaskini, magonjwa kama ukimwi, kifua kikuu na malaria, vifo vya kinamama wakati wa kujifungua na mifarakano katika ndoa.

Japo huenda kuna sababu lukuki zinazobabisha baadhi ya mikoa kuwa na yatima wengi, Mwananchi limebaini kuwa mikoa mitatu inayoongoza kuwa na yatima wengi katika shule za msingi ya Iringa, Njombe na Mbeya pia inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa viashiria vya Ukimwi na Malaria (THMIS) wa mwaka 2011/12.

Njombe inaongoza kwa kuwa na watu wengi wenye virusi vya ukimwi kwa kuwa na asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mbeya kwa asilimia tisa. Ikumbukwe kuwa wakati huo, wastani wa kitaifa wa watu wenye VVU ulikuwa  ni asilimia 5.1.

Changamoto za wanafunzi yatima

Tofauti na watoto wenye wazazi wote, yatima hukabiliwa na changamoto lukuki kutokana na baadhi kukosa walezi imara na wenye mapenzi mema, jambo linalofanya wakose haki zao na fursa nyingi za kujiendeleza.

“Tafiti zinaonyesha kuwa yatima huwa na changamoto za kifedha na vikwazo vingine vya kupata elimu, hivyo huwa katika hatihati ya kukosa elimu bora ambayo ingewapa fursa ya kujikita kwenye taaluma zinazohitaji ujuzi wa juu na kupata ajira zinazolipa zaidi,” anasema mtafiti wa Save the Children, Anitha Martine.

Mbali na elimu,  anasema yatima wapo hatarini kupata msongo wa mawazo na matatizo ya kisaikolojia kutokana na kukosa malezi kikamilifu, hasa wale wasiokuwa na walezi wa uhakika na kufanya watoto hao washindwe kufurahia utoto wao na kuishi kwa afya.   

Watoto wengi yatima wamekuwa wakinufaika na fursa za elimu katika shule mbalimbali nchini. Picha ya Maktaba
Watoto wengi yatima wamekuwa wakinufaika na fursa za elimu katika shule mbalimbali nchini. Picha ya Maktaba

Martine ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya watoto, anasema yatima pia hukumbana na changamoto ya ulinzi katika familia na jamii, jambo linalowafanya wawe waathirika wakubwa wa mimba na ndoa za utotoni ambazo huwakosesha pia fursa za kimasomo.

Hata hivyo, watoto hawa wanaweza kulelewa katika mazingira mazuri ambayo yatawafanya wapate fursa nyingi kama wenye wazazi wote wawili.

Mkurugenzi wa huduma za watoto wa shirika lisilo la kiserikali la C-Sema, Emmanuel Michael anasema kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii ili iweze kutambua umuhimu wa haki na ustawi kwa watoto  yatima na namna ya kuwalea  kama watoto wengine.

“Hii itasaidia watoto hawa waweze kukua na kutimiza ndoto zao na kujenga jamii yenye usawa,” anasema.

Hata hivyo, anasema jamii pekee haitafanikiwa kama hakutakuwa na utekelezwaji wa sheria, sera na miongozo mingineyo inayohusu maslahi na ustawi wa watoto kama vile sheria ya mtoto.

“Ni lazima kurekebisha sheria hasa zile ambazo zinamkandamiza mtoto kama vile sheria ya ndoa, ambayo kwa namna moja inaweza kuchangia kwa watoto yatima hasa wale wa jinsia ya kike kujikuta wakikumbwa na janga la ndoa na mimba za utotoni,” anasema.

Ili kuwasaidia watoto wakiwamo yatima iwapo wamekumbwa na masaibu ya kuvunjiwa haki wakiwa shule au maeneo mengine, Michael  anawaomba wananchi kupiga simu namba 116 ambayo ni ya bure.

Yatima na elimu

Serikali katika ngazi mbalimbali imesema inachukua hatua ya kuwatambua na kuwalinda yatima, ikiwamo njia mahususi ya kuwatambua iliyosaidia hadi kupatikana kwa takwimu za wanafunzi yatima shuleni.

Katika mkoa wa Mbeya ambao ni wa tatu kwa kuwa na yatima wengi katika shule ya msingi, kuna mpango wa kuanzisha mfuko wa elimu wa mkoa unaolenga kuwawezesha wanafunzi wote wanaosoma katika mazingira magumu hususan yatima.

Mkoa huo ulikuwa na yatima 41,956 mwaka jana kati ya wanafunzi 181,845 ambao ni sawa na asilimia 12.7 ikiwa ni mara moja na nusu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 8.5 ya yatima waliopo katika shule za msingi za umma na zile zisizo za Serikali.

Ofisa elimu wa Mkoa wa Mbeya, Paulina Ndigeza, anasema yatima ni wengi katika mkoa huo kiwango ambacho huenda kikazidi hata takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya  Rais-Tamisemi mapema mwaka huu, jambo lililofanya watafute njia ya haraka kuwasaidia.

Hadi sasa, Ndigeza anasema kuna utaratibu wa kuwasaidia watoto yatima kupitia halmashauri ambazo huwatambua waliopo na kuwawezesha, ili waweze kuendelea kimasomo na kupata fursa nyingine muhimu za kimaisha.

Hata hivyo, mamlaka za Serikali za Mitaa pekee haziwezi kutatua changamoto zinazowakabili, ili kuwafanya yatima wapate fursa sawa na wale wenye wazazi wote wawili.

Ili kuwalinda na kuwawezesha watoto wanaoishi katika mazingira magumu, Serikali mwaka huu imeanza kutekeleza mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto utakaotekelezwa  kwa miaka mitano.

Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Erasto Ching’oro anasema malezi ya watoto yatima ni mtambuka kwa kuwa yanahusisha taasisi na watu mbalimbali wakiwamo wanajamii, jambo ambalo linasisitizwa na mpango huo ulioanza Julai.

Ching’oro anasema halmashauri hufanya utambuzi wa yatima wote waliopo shule na wasiokuwepo, familia wanazotokea na mahitaji yao ili kuona namna inavyoweza kuwasaidia ikiwamo katika masuala ya kielimu na pia kuwaunganisha na wadau wengine kama asasi za kiraia wapate misaada zaidi.

“Katika haki tano za msingi kwa watoto, elimu ni moja wapo,  ndiyo maana huwa tunafanya utambuzi katika kila familia ili tujue mahitaji yao na kuangalia namna ya kuwasaidia, ‘’ anasema na kuongeza:

“Nakiri huenda kuna upungufu katika utoaji taarifa za upatikanaji wa huduma zinazotolewa kwa watoto hao kwa wananchi, lakini tunajitahidi  kushirikiana na taasisi mbalimbali  kuwapatia huduma muhimu wanazohitaji.’

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania