Nuzulack Dausen November 21, 2017
- Mkoa huo pia ndiyo unaongoza kwa wanafunzi wengi kuacha masomo elimu ya msingi.
Dar es Salaam. Sophia Mlehela, mkazi wa kata ya Ibondo mkoani Geita anajuta kwa kukaa mbali na mwanaye na kutompa elimu ya maumbile kiasi cha kumfanya apate mimba akiwa mwanafunzi.
Mtoto wa Sophia mwenye miaka 13 amefukuzwa masomo baada ya kujifungilia chooni katika shule ya Msingi Ibondo alikokuwa akisoma na kichanga kufariki dunia.
“Sikujua kama mwanangu ni mjamzito siku zote niko naye lakini sijawahi kumfundisha wala kumweleza kuwa na kupata mimba au magonjwa kama atajiingiza kwenye uhusiano,” amenukuliwa Sophia na Mwananchi leo Alhamis Novemba 21.
“Niliamini bado ni mdogo hata alipopata ujauzito hakuonyesha na alifanya shughuli zake kama kawaida.”
Mtoto wa Sophia aliyeachishwa masomo kutokana kutokana tukio la kujifungua mtoto ni miongoni mwa maelfu ya wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari nchini ambao husitisha ndoto zao za kielimu kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, mimba, na wachache sana kutokana na vifo.
Hata hivyo, tukio hilo lililotokea huko mkoani Geita siyo bahati mbaya. Mkoa wa Geita kwa mujibu wa takwimu za msingi za elimu za Tanzania (Best) mwaka 2015, unaongoza kwa wanafunzi kuacha masomo katika elimu ya msingi baada ya watoto 10,044 kuacha masomo mwaka huo.
Geita inafuatiwa kwa karibu na Tabora, Tanga, Kagera na Simiyu zenye wanafunzi zaidi ya 7,000 walioacha masomo ndani ya mwaka mmoja.
Mkoa wa Njombe ndiyo ulikuwa na kiwango kidogo cha wanafunzi walioacha masomo mwaka juzi baada ya kuwa na watoto 126 tu ikifuatiwa na Iringa, Ruvuma na Kilimanjaro.
Kitaifa, mwaka huo wanafunzi 85,985 waliacha masomo ya elimu ya msingi huku wengi zaidi wakiwa ni wa darasa la tatu na la sita waliozidi watoto 15,000 kila moja.
Madarasa hayo mawili kwa pamoja yalikuwa na asilimia 38 ya wanafunzi walioacha masomo mwaka huo katika elimu ya msingi sawa na watoto wanne kwa kwa kila kumi.
“Idadi ya walioacha masomo ilikuwa kubwa zaidi katika darasa la tatu na la sita kuliko madarasa mengine na sababu kubwa zaidi ya hali hiyo ni utoro na nyingine ni vifo, mimba na ukosefu wa mahitaji ya msingi,” inasomeka sehemu ya ripoti ya takwimu hizo za Serikali kuhusu wanafunzi wanaoacha masomo ya elimu ya msingi.
Utafiti wa Uwezo wa mwaka 2015 uliochapwa katika tovuti ya takwimu huru ya Hurumap Tanzania ulibaini kuwa takriban watoto wanne kwa kila 100 wenye umri wa miaka saba hadi 16 walikuwa wameacha masomo.
Juni mwaka jana Serikali ilifanya mabadiliko ya sheria ya elimu sura 353 kwa kuwabana zaidi wanaume wakware wanaowapatia mimba wanafunzi kwa kuweka adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa atakayebainika na mahakama kufanya kitendo hicho.
Awali adhabu hiyo ilikuwa ni ndogo kwa mtu anayetiwa hatiani kumtia mimba binti alikuwa anatakiwa kulipa faini ya Sh500, 000 au jela miaka mitatu kwa kosa la pili jambo ambalo wadau wakiwemo wabunge walisema ni adhabu ndogo.
Wadau wa elimu wamekuwa wakiishauri Serikali mara kwa mara kuwadhibiti wanaowapatia mimba wanafunzi kama ilivyotokea kwa mtoto wa Sophia kwa kuwapatia adhabu kali na kuwawekea mazingira mazuri ya kusomea yatakayopunguza vishawishi.
Mdau wa elimu, Alistidia Kamugisha anasema ili kupunguza tatizo la wanafunzi kuacha masomo ni vyema Serikali na wadau wakawekeza zaidi kwenye utoaji wa chakula shuleni, kujenga mabweni na uanzishaji wa shule za pembezoni (satellite schools) na utoaji wa elimu ya afya ya uzazi kuepusha mimba za utotoni.
Soma zaidi: Walianza shule 103 wakahitimu saba tu!
“Shule nyingi hazitoi chakula cha mchana wala uji, watoto wengi wanataabika kwa njaaa unakuta mtoto nyumbani usiku hakula chakula cha kutosha, asubuhi hapati kifungua kinywa na anashinda hivyo hivyo hadi jioni atakapo rudi nyumbani,” anasema Kamugisha.
“Wengine wanatembea mwendo mrefu kilometa tano hadi sita au na zaidi na pengine nyumbani chakula hakuna hivyo uwepo mkakati wa makusudi wa kupatikana chakula mashuleni kwa kuhamasisha wazazi kuchangia,” anaongeza.
Kamugisha anatolea mfano wa shule ya msingi Chumo wilayani Kilwa ambayo wanafunzi hutembea zaidi ya kilometa tano na asubuhi wanakuwa wamekula kiporo cha ugali wakifika njiani wanautapika, tabu ambazo haziwezi kumvutia mtoto kuipenda elimu.
Anasema shule zijitahidi kurudisha hadhi zao kama zamani na viongozi wafuate ushauri wa wataalamu wa elimu wa kuboresha mazingira kiasi cha kuwafanya wanafunzi wajisikie kuipenda kila wakati.
“Makabila ambayo bado yana mila za kuchezwa ngoma watoto wanawafundisha watoto mambo ya ngono mapema jambo linalosababisha kujiingiza kwenye mapenzi hivyo ni lazima elimu iendelee kutolewa ili kuachana na mila potofu,” anasema Kamugisha.
Februari mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa wilaya ya Hanang katika ziara mkoani Manyara alieleza kuwa Serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa kike ili wapate haki ya elimu na kuhakikisha wanakamilisha ndoto zao za kielimu hadi chuo kikuu kwa kujenga mabweni na kuwapatia adhabu kali wanaowapatia mimba wanafunzi.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.