Yanayofahamika kuhusu ukuaji wa elimu ya msingi Tanzania

Nuzulack Dausen
December 5, 2017

 

  • Kuna mafanikio makubwa katika uandikishaji wa wanafunzi.
  • Bado serikali inatakiwa kuwekeza katika njia madhubuti zitakazowasaidia watoto kujifunza

[email protected]

Dar es Salaam. Baada ya kuporomoka kwa kasi miaka minne iliyopita, ufaulu wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) umeendelea kupanda kutoka wanafunzi 57 kwa kila 100 waliofanya mtihani huo mwaka 2014 hadi wanafunzi 73 mwaka huu.

Kasi hiyo ya ufaulu ni kubwa ikiwa ni ukuaji wa asilimia 28 ndani ya miaka minne huku mafanikio makubwa yakionekana zaidi mwaka 2015.

Hata pamoja na mafanikio hayo kwa jicho la ufaulu, kuna mambo mengine ya kuyatizama katika safari ya uboreshaji wa elimu ya msingi nchini ambayo inakumbwa na changamoto lukuki kiasi cha kupunguza ufanisi wa wanafunzi kujifunza.

Miongoni mwa mambo ya msingi ya kuyaangazia ni pamoja na uandikishaji wa wanafunzi, uwepo wa walimu wa kutosha na vyumba vya madarasa, wanaojiunga na utekelezaji wa bajeti ya elimu na wale wanaojiunga kidato cha kwanza kutokana elimu ya msingi.

Uandikishaji wa wanafunzi

Katika nchi yeyote ulimwenguni, elimu ya msingi ni nguzo muhimu ya kujenga maarifa kwa jamii ili kuchochea maendeleo na moja ya malengo ya Serikali na Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha hakuna mtoto ambaye anaachwa nyuma kupata elimu.

Ndani ya kipindi hicho cha miaka minne, idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 5.1 kutoka wanafunzi milioni 8.22 mwaka 2014 hadi wanafunzi milioni 8.63 mwaka jana kwa mujibu wa takwimu za msingi za elimu za Tanzania (Best) mwaka 2016.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya ongezeko hilo la wanafunzi lilishuhudiwa mwaka jana shukran kwa sera mpya ya Serikali ya rais John Magufuli iliyoanza kutekeleza sera ya elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne.

 

“Hii imechangiwa zaidi na ongezeko la aundikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kutoka na sera ya elimu bure. Pia, uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya wazazi, mashirika ya kidini, na mashirika ya kiraia katika utoaji wa elimu ya msingi nchini,” inasomeka sehemu ya ripoti ya takwimu za Best 2016 iliyotolewa mapema mwaka huu.

Pamoja na mafanikio hayo na wito wa lengo la nne la malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) la kutomuacha mtoto yeyote nyuma, bado kuna watoto 14 kati ya 100 (asilimia 14.2) wenye umri wa kwenda shule nchini (miaka saba hadi 13) hawapo shule jambo linaloonyesha hitaji la kuihamasisha jamii kuwapeleka watoto shule.

Ripoti ya Best inaeleza kuwa mbali na kutoa elimu bure, kuna haja kuanzisha mikakati mahsusi kama kutoa chakula bure kwa wanafunzi ili kuwavutia wengi hususan kutoka kwenye familia maskini.

Wachambuzi wa masuala ya elimu wanaeleza kuwa ujenzi wa shule karibu na makazi ya watu na utoaji wa chakula shuleni utafanya watoto wanaotoka mbali na shule kutoshinda na njaa.

 

Changamoto ya walimu

Hata hivyo, kasi ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi nchini haiendani na ile ya walimu wanaotakiwa kuwapa maarifa.

Hadi mwaka jana, takwimu za Serikali zinaonyesha kitaifa kwa shule za umma na zisizo za Serikali za msingi mwalimu mmoja anafundisha wastani wa watoto 43. Hii ni takriban na uwiano unaotakiwa wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40.

“Asilimia 86.5 ya walimu wana sifa za Ngazi A ambacho ni kiwango cha chini kwa walimu wa msingi. Katika ngazi za elimu ya uzamivu na Stashahada ya juu kuna walimu 131 ambao ni sawa na asilimia 0.1 ya walimu wote,” inasomeka sehemu ya ripoti ya Best.

Hata hivyo, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kwa shule za umma upo juu zaidi kwa mwalimu mmoja kufundisha hadi wanafunzi 48 kwa takwimu za Ofisi ya Rais-Tamisemi za hadi Machi mwaka jana.

Pamoja na takwimu hizo kuonyesha kuwa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi ni mzuri MwananchiData ilibaini kuwa mgawanyo wa watumishi hao katika baadhi ya maeneo hauzingatii mahitaji husika hivyo kufanya maeneo ya vijijini kukosa walimu.

Pia, itakumbwa kuwa walimu ni moja ya watumishi wa umma wengi waliokumbwa na fagio la vyeti feki nchini ambalo lililoondoa takriban watu 10,000 serikalini hivyo kuongeza zaidi mahitaji.

 

Wanaojiunga na kidato cha kwanza

Kumaliza darasa la saba ni jambo moja lakini kuendelea na masomo ya sekondari ilikuwa ni moja ya kikwazo kikubwa kilichokuwa kikifanya sehemu kubwa ya watoto kutotimiza ndoto zao.

Hadi mwaka mwaka 2000, ni wanafunzi 22 tu kwa kila 100 waliomaliza masomo ndiyo walikuwa wakipata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari.

Kwa wakati huo, kiwango hicho kilikuwa kikubwa ikilinganishwa na mwaka 1992 ambapo ni wanafunzi 13 tu kwa kila 100 waliokuwa wakienda kidato cha kwanza.

Takwimu za Best 2016 zinaonyesha mafanikio makubwa yalianza kuonekana zaidi mwaka 2006 baada ya idadi ya wanaojiunga kidato cha kwanza kupaa hadi theluthi mbili ya waliohitimu (asilimia 67.5) kutoka nusu ya wanafunzi (asilimia 49.3) mwaka 2005, shukran kwa uanzishwaji wa shule za sekondari za kata.

Kwa bahati mbaya kiwango cha wanaojiunga na kidato cha kwanza iliporomoka hadi wanafunzi watano kwa kila 10 (asilimia 52) mwaka 2013 kutoka takriban saba kwa kila 10 mwaka 2006.

Matumaini mapya yameanza kurudi mwaka 2015 baada tena ya idadi hiyo kupanda hadi wanafunzi saba kwa kila 10 wanaohitimu elimu ya msingi.

Hata pamoja na idadi ya wanaojiunga sekondari ikionekana kupaa kwa kasi kumekuwa na hoja juu ya uwezo wa wanafunzi husika katika kujifunza.

Baadhi ya wachambuzi wanaeleza kuwa baadhi ya wanafunzi wa Sekondari pamoja na kufaulu mtihani wa darasa la saba bado hawawezi kuelewa masuala ambayo walitakiwa kuyajua wakiwa elimu ya msingi.

Mwishoni mwa Oktoba Mwananchi liliripoti juu ya msichana Anna Matonya aliyehoji alifaulu vipi darasa la saba kuingia kidato cha kwanza. Anna alipaswa kuwa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Magaga wilayani Bahi mkoani Dodoma lakini kutokana na kutoelewa chochote alikacha darasa.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti unaopima namna wanafunzi wanavyojifunza wa asasi za kiraia ya Twaweza wa Uwezo 2015, takriban wanafunzi 19 kwa kila 100 wenye umri wa miaka sita hadi 16 ndiyo wana uwezo mkubwa wa kuelewa masomo yote. Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa pia katika tovuti ya takwimu huru ya Hurumap.

Wadau wa elimu wanasema mfumo wa maswali ya kuchagua unaotumika katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ndiyo tatizo linalofanya wanafunzi wafaulu wakati hawana uwezo.

“Unaweza kumkuta mtoto anabuni jibu na kufaulu, ndio maana wanaokwenda sekondari wengi hawana uwezo kama binti huyu amejikuta haendani na wenzake,”anasema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chifutuka, Daniel Mchomvu.

Pamoja na mafanikio hayo ya ukuaji katika elimu ya msingi, bado Serikali inapaswa kutafuta suluhu ya kuongeza uelewa kwa wanafunzi zaidi kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaohudhuria madarasa.

Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu kujifunza toleo la 2008 iliyotolewa hivi karibuni linaeleza kuwa wanafunzi wanaohitimu bila kujifunza kikamilifu huwa na uzalishaji dhaifu hadi wanapoingia katika au katika maeneo mengine ya maisha.

 

 

 

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania