Mwananchi Data

By Nuzulack Dausen

Wakati wa joto la uchaguzi mkuu mwaka jana, miongoni mwa mambo makubwa ambayo wengi walikuwa wakihitaji kutoka kwa Rais wa awamu ya tano ilikuwa ni uboreshaji wa huduma za afya nchini.

Utafiti uliofanywa na asasi ya kiraia ya Twaweza mapema Septemba mwaka jana ulionyesha kuwa asilimia 59 ya Watanzania waliohojiwa walihitaji maboresho makubwa katika sekta ya afya. Udhaifu katika utoaji wa huduma za afya ulikuwa ni tatizo sugu kiasi cha kuzidi ukosefu wa ajira na rushwa.

Sekta ya afya nchini inakabiliwa na changamoto lukuki zikiwemo za uhaba wa vitanda vya wagonjwa, ukosefu wa dawa, utoro wa madaktari na upungufu wa vituo vya afya.

Mfano, ukosefu wa vitanda umesababisha baadhi ya hospitali kulaza wagonjwa wawili au watatu na wengine kulala chini wakati wakisubiri kupatiwa matibabu.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi mwaka 2012, Tanzania ilikuwa inachechemea katika uwiano wa vitanda kwa mgonjwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Hali hiyo ilifanya baadhi ya wananchi kutokuwa na imani kubwa na vituo vya afya vya umma huku wengine wakihaha kupata matibabu katika vituo vya watu binafsi, maduka ya dawa, vituo vya mashirika ya dini au asasi za kiraia

Mwaka mmoja baadaye na baada ya uongozi mpya wa Rais John Magufuli kuingia madarakani, imani ya wananchi juu ya utoaji wa huduma za afya inaanza kurejea.

Idadi ya watu waliokuwa wakiona kuna mfumo mbovu wa utoaji huduma za afya nchini, wanaanza kuona mabadiliko.

Matokeo ya utafiti mwingine uliofanywa na Twaweza mwaka huu na kutolewa mwanzoni mwa Agosti, unaeleza kuwa idadi ya wananchi wanaoikimbilia kupata matibabu katika vituo vya afya vya umma baada ya kuugua imezidi kwa 15% kutoka mwaka 2015.

Je, nini kimewabadilisha wananchi hao?

Mapema baada ya Rais Magufuli kungia madarakani Novemba mwaka jana, moja ya mambo ya awali ambayo alitaka yafanywe kwa haraka ni kuongeza uwajibikaji katika utumishi wa umma.

Kurudisha hali hiyo, alifanya ziara za kushtukiza katika taasisi mbalimbali za umma na miongoni mwao ilikuwa ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Katika ziara hiyo, Rais alikutana na changamoto lukuki zinazoikabili hospitali hiyo zikiwemo ubovu wa mashine za MRI na CT-Scan na baadhi ya wagonjwa wakilala chini kwa kukosa vitanda.

Matokeo na maagizo kutoka katika ziara hizo yaliamsha ari baada ya Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na naibu wake Hamis Kigwangalla nao kuendeleza ziara katika baadhi ya hospitali jijini Dar es Salaam na mikoani.

Utoro wa madaktari nao unaonekana kupungua. Asilimia 18 ya wananchi waliohojiwa walibainisha kutowakuta madaktari katika vituo vya afya walivyokuwa wameenda kutibiwa kikiwa ni kiwango cha chini takriban mara mbili na nusu ya kile cha mwaka jana.

Pamoja na kukua kwa mtazamo chanya katika huduma za afya nchini, bado sekta hiyo ina changamoto lukuki. Miongoni mwa changamoto hizo ni uhapa wa vituo vya afya na wahudumu. Twaweza wanabainisha kuwa yanahitajika mabadiliko makubwa katika mfumo wa kibajeti hususan kuongeza uwekezaji katika dawa na vifaatiba.

Wakati wa kampeni Rais Magufuli aliahidi kuendeleza sera ya kujenga Zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata, hospitali kila wilaya na mkoa pamoja na kuboresha huduma za upatikanaji wa dawa na vifaatiba.

Lakini bado tatizo la uhaba wa dawa limeendelea kushamiri. Katika utafiti huo wa Twaweza uliofanywa Tanzania bara, idadi ya wagonjwa walioenda katika vituo vya afya na kukosa dawa au vifaatiba nayo imeongezeka.
Ripoti inaonyesha kuwa asilimia 59 ya wananchi walikosa dawa au vifaatiba tofauti na asilimia 53 mwaka jana.

Pia, tatizo sugu la ukosefu wa vitanda bado linaendelea. Mwaka huu katika utafiti huo wa Twaweza, ilibainishwa kuwa watu takriban wanne kati ya 10 walishuhudia mtu akitakiwa kulala kitanda kimoja na mwingine tofauti na watu watatu kati ya 10 mwaka jana.

Waziri Ummy Mwalimu alilieleza Bunge wakati akisoma bajeti yake mapema mwaka huu kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika ununuzi wa dawa na vifaatiba.

Katika mwaka wa fedha wa 2016/17, Serikali imetenga Sh65.5 bilioni takriban mara mbili ya fedha zilizotengwa mwaka jana ambazo zilikuwa Sh37 bilioni.