Mapato ya hisa yashuka kwa asilimia 68

Nuzulack Dausen
August 11, 2017

Ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa DSE umepanda kwa Sh300 bilioni

Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mapato yatokanayo na mauzo ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) yameporomoka kwa asilimia 68 licha ya wawekezaji wa nje kuvutiwa na hisa za kampuni tatu.

Takwimu za DSE zinaonyesha kuwa Sh4 bilioni zilipatikana wiki iliyoishia Agosti 4, ikilinganishwa na Sh12.5 bilioni zilizopatikana Julai 28.

Hata hivyo, kampuni za TBL, TCC na CRDB ziling’ara wiki iliyopita kutokana na kuvutia wawekezaji wengi wa nje wanaotarajia kwamba zitaendeleea kufanya vizuri na kuwapatia gawio mwishoni mwa mwaka.

Habari inayohusiana: Mauzo ya hisa yaporomoka DSE

Katika wiki hii ya kwanza ya Agosti, kampuni iliyoongoza kwa mauzo ni TBL kwa asilimia 94.77, TCC asilimia 2.89, na Benki ya CRDB asilimia 1.53.

“Kawaida, wawekezaji wa nje wanamatumaini kuwa kampuni hizo zitaendelea kufanya vizuri hivyo kuwapatia gawio la kutosha,” alisema ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Zan Securities, Raphael Masumbuko.

Kupungua kwa mapato kunatokana na kushuka kwa hisa zilizouzwa kwa asilimia 98.7 hadi kufikia 600,000 wiki iliyopita kutoka milioni 46 zilizouzwa wiki iliyoishia Julai 28.

Hata hivyo,ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa DSE umepanda kwa Sh300 bilioni, kutoka Sh17.9 trilioni wiki iliyoishia Julai 28 hadi Sh18.3 trilioni wiki iliyoishia Agosti 4.

Taarifa ya soko la hisa inaeleza ongezeko hilo la mtaji linatokana na kupanda kwa bei ya hisa za Kampuni ya Nation Media Group (NMG) ambazo zimepanda kwa asilimia 11.9.

NMG ni kampuni mama ya Mwananchi Communications Limited, wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Kampuni nyingine zilizochangia kukua kwa mtaji huo ni Kampuni ya bia ya Afrika mashariki (EABL) ambayo imepanda kwa asilimia 2.5.

Benki ya KCB imepanda kwa silimia 2.35 na Kampuni ya Uchimbaji wa madini ya Accacia asilimia 2.2.

Hisa za NMG kwa wili iliyoishia Julai 28 zilikuwa zinauzwa Sh2,360 lakini Agosti 4 zilikuwa zinauzwa Sh2640, EABL hisa zake ziliuzwa Sh5,580 Julai 28 lakini Agosti 4 ziliuzwa 5,720.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania